Mkasa wa mwanamuziki Harmonize nchini Kenya

0

Mwanamuziki kutoka Tanzania Rajab Abdul maarufu kama Harmonize, alikamatwa na polisi kisha kuachiwa huru Nairobi nchini Kenya kwa madai ya kulipwa bila kutokea katika baadhi ya kumbi za starehe kwa ajili ya kutumbuiza.

Kwa mujibu wa vyombo vya Habari nchini Kenya Harmonize kwa ushirikiano na mwenyeji wake msanii wa Vichekesho Erick Omondi wa nchini Kenya, walitoa ahadi ya kutumbuiza lakini jambo hilo halikufanyika.

Baada ya madai hayo, aliyekua gavana wa Nairobi Mike Sonko ambaye alimualika pia Harmonize kutumbuiza mjini Mombasa alisema kuwa Harmonize ameachiwa, na sasa anaelekea Mombasa.

‘’kuna klabu alitakiwa kutumbuiza lakini hakwenda, sio yeye aliosaini mkataba bali ni madalali, na sasa yupo huru na anelekea Mombasa kutumbuiza mashabiki wa Mombasa’’ anasema Sonko

Katika ukurasa wa mchekeshaji Erick Omondi, anadai kuwa alifika mapema leo katika kituo cha polisi cha Kileleshwa jijini Nairobi ili kumuwekea dhamana Harmonize lakini aliishia kupigwa ngumi ya uso na msanii huyo.

Kwa madai ya Omondi alimshauri Harmonize arudishe pesa kwa wamiliki wa kumbi za starehe lakini Harmonize alikataa.

Baadhi ya wamiliki wa kumbi za starehe wanatupa lawama kwa Harmonize pamoja na Erick Omondi.

‘’timu yote wanatakiwa kulaumiwa, Harmonize na Omondi, tumelipia pesa lakini hatujapata huduma, mimi Pamoja na mashabiki, na mkataba unasema anatakiwa kutumbuiza kwa saa moja na nusu, lakini hilo halikutokea’’ anasema mkurugenzi wa kumbi ya starehe ya Captain Lounge.

Kwa upande wa meneja wa Harmonize anayejulikana kama Mchopa, anasema hajapata taarifa za kukamatwa kwake ila anawatafuta Harmonize na timu yake walioko nchini Kenya lakini hawapatikani’’

‘’Inawezekana wapo kwenye ndege ndio mana hawapatikani’’ anasema Mchopa.

Leave A Reply

Your email address will not be published.